1985 - 2007

 

Maswali Yaulizwayo Mara Kwa Mara

Kijitabu cha maelekezo kwa wanafunzi, viongozi wa kozi, na wachungaji

Karibu Kwenye Shule Ya Umisheni Katika Lugha Ya Kiswahili
Support Pages in English

 

Maswali Yaulizwayo Mara Kwa Mara

Kijitabu cha maelekezo kwa wanafunzi, viongozi wa kozi, na wachungaji


Kuhusiana na masomo yanayotolewa bure na DCI kwa ajili ya Shule za Umisheni.
Tunayo majibu ya kila swali.

 

Mtandao wa Shule ya Umisheni ya DCI
© 1985-2007 The DCI Foundation England
Kwa kushirikiana na makanisa na madhehebu ulimwenguni kote

 

 

Yaliyomo

Namna gani unaweza kujiunga au kuanza, gharama zake, na je, masomo yanapatikana  kwa njia ya Posta?

Je, yawezekana kupokea au kutoa Stashahada?

Kwa Wachungaji, Viongozi na Wasimamizi

Je, Shule ya Umisheni inawezaje kufanya kazi kwa viwango vizuri?

Kwa namna gani unaweza kuanzisha shule yako mwenyewe?

Na mengineyo, kama vile, Sisi ni akina nani, n.k.

 

1. KWA WANAFUNZI MMOJA MMOJA NA WATU BINAFSI WANAOPENDA KUJISOMEA NYUMBANI

 

Je, nitaanzaje? Na masomo haya yanagharimu fedha kiasi gani?

Hakuna hata kidogo. Ni bure, hakuna mtego, hakuna kuchapisha kidogo, hakuna kadi ya mkopo. Ni bure.

Masimulizi haya kuhusu Shule ya Umisheni na muda wetu wa kukusaidia wewe ili uweze kuanza ni bure. Masomo kama haya yanapotolewa na taasisi nyingine nchini Uingereza yanagharimu si chini ya £2,500 sawa na $4,000 na kiasi hiki ni mbali na gharama za malazi na chakula. Kwahiyo unaweza kuona thamani ya zawadi hii ya bure. Kwa wakati wo wote ule hutaona mtu ye yote kutoka taasisi ya DCI akidai kwako fedha, namba za kadi yako ya mkopo, hundi, au ada kwa ajili ya masomo haya. Wakifanya hivyo, basi ujue hao hawatokani na taasisi ya DCI, na wewe usifanye malipo yo yote kwa ajili ya masomo haya.

 

Je, mnaweza kunitumia masomo haya kwa njia ya posta?

Samahani sana hatutaweza kufanya hivyo kwa sababu ya gharama kubwa iliyopo ya kuchapa na kutuma kwa njia ya posta maelfu kwa maelfu ya vifurushi vyenye masomo haya; na tusingeweza kutoa kozi hii bure bila malipo. Wewe unaweza kuyapata masomo haya yote katika kipindi cha dakika 10 tu na kisha ukaendelea kuyachapisha somo moja baada ya lingine kwa wakati wako na kwa kadiri ya mahitaji yako.

 

Je, ninaweza kusoma kwa njia ya mawasiliano?

Tunasikitika kwamba hilo halitawezekana kutokana na ukubwa wa shughuli yenyewe; kupokea maelfu kwa maelfu ya masomo kutoka ulimwengu mzima si kazi ndogo. Jawabu ni kwa wewe kumpata msimamizi katika eneo unaloishi; angalia maelezo hapo chini.

 

Je, kuna ulazima wa kujiandikisha?

Hapana, hakuna ulazima. Hapahitajiki fomu ya maombi, nasi tutakupokea wewe kama mwanafunzi wetu na kukusaidia. Masomo haya ni kutoka kwenye Shule ya Umisheni na ya awali iliyoanzia nchini Uingereza. Masomo haya yanatolewa bure bila malipo kwa kila mtu; watu wa marika yote, wake kwa waume, maskini au tajiri, walio vijana au wazee; watu wa rangi zote na bila kujali usuli wao. Kozi hii ni zawadi yetu kwako. Masomo haya yanafundishwa pia katika makanisa yaliyo mengi na madarasa ulimwenguni pote.

 

Nifanye nini cha kwanza katika kila somo?

Alimradi kazi inakamilika, haidhuru kitu unaanzia wapi na kuishia wapi. Mtaala mkuu katika kila ukurasa ni kukufanya wewe utafiti na kuwaza kuhusu somo hilo. Kisha tunatilia mkazo somo kwa kukupa maandiko ya kusoma na pia mazungumzo. Tunakupa kazi ya kuandika insha fupi na tunakutaka ufanye mazoezi na hayo yatakufanya uwe na uzoefu mzuri wa yale unayojifunza.

 

Anza kila somo kwa namna inayokupendeza wewe; lakini ukitaka tunaweza kupendekeza mpangilio ufuatao:

 1. Soma mistari ya Biblia ili kuweka sawa muktadha.

 2. Somo lenyewe.

 3. Kariri mstari uliopewa.

 4. Tafakari mstari uliopewa.

 5. Kazi ya kuandika.

 6. Kazi ya vitendo.

 7. Mazungumzo.

 8. Usisahau vipindi viwili vya maombi; wakati wa kuanza somo, na wakati wa kumalizia.

 

Tafadhali zingatia kwamba kama unajisomea kozi hii peke yako, jambo ambalo ni zuri, pana baadhi ya mambo ambayo hutaweza kuyafanya kwa sababu yameandaliwa kwa ajili ya kikundi, kwa mfano pale panapoagizwa kufanya mazungumzo. Pengine familia yako na rafiki zako watafurahia kusikia kutoka kwako yale uliyojifunza. Hulazimiki kufanya kila jambo mara moja, somo linaweza likachukua hata wiki moja kumalizika.

 

Je, naweza kuchagua sehemu moja tu ya kozi hii na kuisoma?

Ndiyo, unaweza; tafadhali jichagulie kiasi cho chote cha masomo na usome kwa uhuru kama upendavyo. Wewe anzia sehemu yo yote inayokupendeza zaidi. Ukitaka fuata utaratibu wetu, uamuzi ni wako. 

 

Je, ninalazimika kufanya mazoezi yote kwa vitendo na kazi za kuandika?

Hapana, hulazimiki, ila ukiamua kufanya mazoezi hayo utanufaika zaidi. Baadhi ya watu hupenda kusoma tu sehemu kuu kwa ajili ya ibada binafsi. Wakati mwingine baadhi ya watu wanashindwa kuandika vema kwa Kiingereza, au hata kwa lugha yao wenyewe. Na katika nchi nyingine kama wanafunzi watajaribu kufanya mazoezi kwa vitendo wataishia jela; na sisi hatutaki hilo litukie.

Njia mbadala ni kumwona Mchungaji wako na kumwomba akupe nafasi kanisani kwake katika eneo linalofanana na hilo unalotaka kufanyia mazoezi. Masaa mawili kwa kila somo ni muda wa kutosha. Kama unawania cheti, basi ni vema utunze orodha ya kazi zote unazozifanya na muda unaotumia kuzifanya. Hili lilikubalika katika shule yetu wenyewe.

 

Je, ninahitaji kununua vitabu na vitagharimu bei gani?

Kitabu pekee utakachokihitaji ni Biblia iliyoandikwa kwa lugha yako.

 

Je, itanichukua muda gani kuimaliza kozi hii?

Tunapendekeza kwamba masomo yote, mazoezi ya vitendo na ya kuandika yakamilike katika kipindi kisichozidi miaka miwili; ni muda wa kutosha kabisa. Watu wengi hufanya somo moja kwa wiki moja na kukamilisha kila kitu vizuri. Lakini wengine wanahitaji siku tatu au nne tu kukamilisha kazi yote. Haifai kumaliza somo moja kwa siku moja; huko kutakuwa ni kukariri kusikokuwa na manufaa ya muda mrefu. Utahitaji muda wa kutosha kupitia maandiko na kuruhusu yapitie akilini mwako, na kuwa na mizizi moyoni mwako na rohoni mwako. Pia utahitaji muda wa kufanya mazoezi. Hakuna faida ya kupitia masomo haya harakaharaka halafu ukatazamia kupata wafuasi.

 

Je, naweza kupata stashahada?

Mnaweza kunipa stashahada kutoka Uingereza?

Tunasikitika kwamba hatutaweza kufanya hivyo; awali tulijaribu kutoa stashahada lakini pakaonekana ugumu wa kuhakiki maombi ya maelfu ya wanafunzi kutoka ulimwenguni kote. Tutakuonesha namna ya kupokea au kutoa stashahada katika eneo lako. Angalia sehemu maalum yenye maelezo kuhusu stashahada hapo chini.

 

Je, nawezaje kupokea stashahada?

Hakuna ugumu wo wote. Kwa mfano, makanisa yaliyo mengi, misheni na Shule za Biblia zinazofundishia masomo yetu, hutoa stashahada zao kwa  wanafunzi wanaofaulu vizuri. Stashahada hizo hukubalika na makanisa, mamlaka, waajiri na maafisa katika maeneo yao kwa sababu zinaweza kuhakikiwa kirahisi.

 

HATUA YA KWANZA: Ikiwa kweli unataka kusoma na kupitia kila eneo la masomo haya na kufanya mitihani, na ikiwa unataka kupokea stashahada, basi ni vema kabla hujaanza uonane na Mchungaji wako, au kiongozi wa kanisa, misheni, kanisa la nyumbani, au kiongozi wa shule. Ongea naye uone kama atakuwa tayari kukupa stashahada iwapo utasoma kozi hii chini ya uangalizi na kufaulu vizuri. Wachungaji na viongozi walio wengi watakuwa tayari kumsaidia mtu aliye na kiu ya kujifunza neno la Mungu. Makanisa na Shule za Biblia watapenda sana kutumia masomo haya kufundishia katika taasisi zao mara watakapong’amua uzuri wake.

 

HATUA YA PILI: Unatakiwa kumpata msimamizi halali atakayesoma na kusahihisha kazi zako za kuandika, atakayesikiliza taarifa zako kuhusu mazoezi ya vitendo, atakayezungumza nawe na kutunza kumbukumbu zako. Yeye ndiye atakayewasilisha matokeo yako kwa mchungaji au kiongozi.

 

HATUA YA TATU: Mwishoni mwa masomo yako ni lazima kazi yako na taarifa za msimamizi wako vihakikiwe na ama kanisa lako, au kiongozi wa umisheni au mtu mwingine ye yote wa fani hiyo. Ikiwa kazi yako itakidhi viwango, kanisa au taasisi husika itakupa stashahada kama sehemu ya huduma ya Jumapili au katika kusanyiko la kanisa la nyumbani. Mara kwa mara makanisa na Shule za Biblia wana utaratibu maalum wa kuwafanyia Sherehe za Mahafali wanafunzi wao.

 

Ni nani anayeweza kuwa msimamizi wangu?

Tunapendekeza kwamba msimamizi atokane na mojawapo ya makundi yafuatayo: wachungaji, wazee wa kanisa, wachungaji wasaidizi, wamishenari, viongozi wastaafu wa kanisa au wa umisheni, wazazi, viongozi wa makanisa ya nyumbani na wale waliostaafu alimradi wawe ni waamini waliokomaa, wanaowajibika, watu wanaojistahi, wenye kuijua Biblia na walio tayari kutumia muda wao kuzungumza na mwanafunzi na kuomba pamoja naye. Sisi tunafikiri mtu mmoja anaweza kuwahudumia wanafunzi sita. Angalia sehemu inayofuata, inahusiana na wasimamizi. Ukiweza kuwapata rafiki zako wachache mkasoma kwa pamoja, na mtu mwenye uwezo wa kuwasimamia, basi tayari mmekwishaanzisha Shule ya Umisheni, na mnaweza kujipatia stashahada zenu. Angalia sehemu iliyoko hapa chini kwa ushauri kuhusiana na jambo hili.

 

 

2. KWA WACHUNGAJI, VIONGOZI NA WASIMAMIZI; MAALUM KWA MASOMO YA SHULE YA UMISHENI

 

Swali: Ni kwa namna gani Shule ya Umisheni inaweza kufanikiwa?  

Jibu: EAPTC iliyoko Nairobi nchini Kenya ni mfano wa kuigwa.

Wakati mmishenari wa Kikorea Paulo Lee alipofika Nairobi miaka kadhaa iliyopita alianzisha shule ya Biblia, na ingawa ilikuwa nzuri, lakini haikuweza kukidhi matarajio ya idadi kubwa ya wahitimu ambao wangeenda kuanzisha makanisa mapya, na pia kujihusisha na umisheni unaovuka mipaka ya tamaduni mbalimbali.

 

Miaka mitano iliyopita Paulo alibadilisha mambo na akaanza kutumia mfumo wa Shule ya Umisheni ya DCI ambao ni wa kifuasi; na tangu wakati huo wahitimu wamefungua makanisa mapya zaidi ya 60 na shule za umisheni nchini Kenya, zaidi ya 40 nchini Uganda na katika nchi za Burkina Faso, Malawi na Sudan. Shule ya Umisheni nchini Malawi imefanya mahafali yake ya kwanza hivi karibuni, na mmoja wa wahitimu wake yuko kwenye mchakato wa maandalizi ya kufungua Shule ya Umisheni nchini Botswana.

 

Lengo la Paulo Lee ni kufungua makanisa mapya 10,000 na Shule za Umisheni katika Afrika na ulimwenguni kwa ujumla. Yuko njiani akitekeleza azma yake hiyo.

 

Hivi ndivyo Shule ya Umisheni ya EAPTC mjini Nairobi inavyofanya kazi:

 1. Maombi kwa kozi inayofuata yanapokelewa.

 2. Unafanyika utaratibu rahisi wa kuwachagua wanafunzi wasiozidi 15 kwa kila kozi.

 3. Shule ya Umisheni hutoa mafunzo haya kwa muda maalum, kila siku kwa miezi sita, na ndani ya chumba cho chote kinachopatikana, na hakuna vifaa vyo vyote vya gharama kubwa vinavyohitajika. Mazingira yenyewe yana mwelekeo wa nje, kuwatazama watu na mataifa yasiyofikiwa bado, na matarajio ni kwamba wanafunzi wengi watakwenda kufungua shule mpya mahali pengine na kuanzisha kanisa katika mazingira yake; la sivyo watarudi makanisani mwao wakiwa wameandaliwa vizuri kumsaidia mchungaji.

 4. Mahafali. Kila mhitimu anayo ruhusa ya kufundisha mahali pengine yale aliyofundishwa. Kwa maana hiyo mwanafunzi anafanyika kuwa mkufunzi. Nakala ya masomo hayo itapatikana kwa bei isiyokuwa ya kibiashara. Huu ndio ufunguo wa kukua.

 5. Wahitimu watarejea kwenye kanisa lao. Kanisa hilo litakuwa ni kanisa mama litakalowatuma hao wahitimu kwenda kuanzisha Shule ya Umisheni mahali pengine mjini au kijijini na hata nje ya mipaka ya nchi.

 

Na kisha utaratibu unajirudia tena. . .

 1. Shule mpya na huru ya Umisheni itatangazwa kwa neno la mdomo.

 2. Maombi yanapokelewa, wanafunzi wanachaguliwa.

 3. Hiyo Shule mpya inafundisha masomo yaliyotajwa hapo juu kwa muda maalum katika kipindi cha miezi 6 hadi 24.

 

Huyo mhitimu amekuwa mkurugenzi/mkufunzi/mchungaji. Mafunzo haya yanayotolewa bila malipo husababisha maombi, kuwafikia watu, ibada na ushirika na haya yanafanywa sehemu ya kanisa jipya linalotegemezwa na kanisa mama.

 

Siku ya Mahafali. Wahitimu wanaruhusiwa kufundisha mahali pengine yale waliyofundishwa.

 

Kwa mara nyingine baadhi ya wanafunzi wanakwenda kuwa walimu/wachungaji.

Kwa njia hii neno la Bwana linaenea sana na kukua katika uweza (Mdo 19:20) na haya ndiyo maono ya Shule ya kwanza ya Umisheni huko Uingereza kunako mwaka 1987.

 

6. Kwa sasa Shule ya Umisheni ya Nairobi inayosimamiwa na EAPTC inafundisha kozi nyingine . . . angalia hatua ya kwanza.

 

Evangelical Alliance for Preacher Training and Commission

c/o GMK, P.O. Box 3774, Nairobi 00506, Kenya. Internet: www.eaptc.org

 

Kutoka kwa Dk. Les Norman, mwanzilishi wa mtandao wa Shule za Umisheni

Iwapo wewe ni kiongozi wa Shule ya Umisheni au kama una wazo la kuanzisha shule na hivyo kujiunga na mtandao, ninakuhimiza kutwaa kwa matumizi na kutohoa mfano huu wa kuigwa kutoka Kenya kwa sababu matokeo yake kwa kweli ni ya kipekee, na nimeyashuhudia kwa macho yangu.

 

Je, kwa namna gani naweza kuanzisha Shule ya Umisheni?

Je, naweza kuanzisha shule mpya kwa kutumia masomo yenu?

Ninayo shule yangu sasa, je, naweza kutumia masomo yenu?

Ndiyo. Masomo yote pamoja na ushauri wo wote utakaouhitaji ni zawadi yetu kwako, bila malipo. Tutafanya kila tuwezalo kukusaidia wewe.

 

Je, nawezaje kutoa stashahada ya kuaminika?

Sehemu inayofuata ni mahsusi kwa ajili ya Viongozi wa Shule ya Biblia, wa Kanisa na wa Umisheni, ambao wamefuatwa na mwanafunzi au msimamizi wake wakiomba idhini na usimamizi wa kozi wanayokusudia kuchukua wakiwa na tumaini kwamba kanisa, misheni, shule au shirika litatoa stashahada mwishoni mwa kozi na baada ya kufanya mtihani.

Ni jambo la kawaida kwamba mwishoni mwa kozi wanafunzi waliofaulu vizuri wanatarajia kupokea stashahada au cheti. Baadhi ya viongozi wangependa pia kuwapa wanafunzi wao tuzo kama njia ya kuwatia moyo kila wanapomaliza sehemu mojawapo ya kozi. Cheti anachopewa mhitimu ni tuzo kwa uvumilivu na bidii yake katika masomo, na pia ni mtaji kwa sababu kinaongezea wasifu wake. Cheti hicho anaweza kukiwasilisha kwa mwajiri wake, uongozi wa kanisa, na hata kwa vyuo vya elimu ya juu.

Ili cheti kiwe chenye heshima na cha kuaminika ni lazima kitolewe katika njia sahihi. Ukurasa huu utausaidia uongozi kuwatunukia wanafunzi wao tuzo za thamani.

Mwanafunzi anapaswa kupewa vitu viwili:

 

Cheti 

Hii ni hati yenye maelezo na uhalali wa cheti chenyewe.

 

Cheti Chenyewe

Usije ukaweka nakala ya vyeti vyako kwenye mtandao wa kompyuta kwa sababu watu wasiokuwa waaminifu watavichapisha na kuviuza mitaani. Hali hiyo itashusha hadhi na thamani ya vyeti vyako.

 

Ni vyepesi kutengeneza vyeti vyako mwenyewe. Kwenye kompyuta unaweza kutumia Microsoft Word, Microsoft Publisher, Corel, Serif na kadhalika. Utapata humo mifano ya vyeti vizuri na vyenye kingo zilizotiwa nakshi kwa matumizi yako. Kazi yako wewe ni kuandika maneno unayotaka na kwa mpangilio ulio chaguo lako, majina ya wanafunzi wako, na kisha kuchapisha, na hasa chapa ya rangi itapendeza zaidi. Cheti hakipaswi kuwa na mambo mengi au cha gharama kubwa. Waweza pia kununua kutoka kwenye maduka ya vitabu na yale yauzayo vifaa vya maofisini, vyeti ambavyo havijajazwa, ikawa kazi yako ni kujaza tu.  

Ukitaka unaweza kuiita tuzo yako Cheti au Stashahada ya Masomo ya Biblia. Tuzo hiyo sharti iwe na vitu vifuatavyo: Jina, uthibitisho kwamba <jina la mwanafunzi wako> amehitimu kozi iliyokuwa na usimamizi mzuri iliyotolewa na Dk L.H. Norman wa Mtandao wa DCI wa Wakristo Ulimwenguni wenye makao yake huko Uingereza, kuanzia <tarehe> hadi <tarehe> na amefaulu mtihani uliotolewa, (na ustahili, au na heshima).

 

Cheti ni lazima kitiwe saini kwa kalamu ya wino na maafisa wawili, kiandikwe tarehe na kupigwa mhuri mbele na nyuma; na ikiwezekana kiwekewe lakiri nyekundu kwa mbele. Cheti kitolewe kikiwa ndani ya kabrasha maalum la kutolea vyeti, au kwenye jalada la plastiki, au kwenye bahasha ili kukihifadhi cheti kisichafuke.

 

Hati Yenye Maelezo

Hii ndiyo inayokipa cheti au stashahada uhalali wake na ni lazima ipigwe chapa kwenye karatasi maalum yenye jina na nembo ya shule. Kila ukurasa wa hati hiyo utapigwa mhuri na kutiwa saini na mchungaji au Mkuu wa Shule. Kinyume cha hayo hati itatiliwa mashaka na bodi yo yote siku za baadaye. Nakala ya pili ya hati hiyo itahifadhiwa na Shule.

 

Hati hiyo inapaswa kuwa na vitu vifuatavyo:

 1. Jina kamili la mwanafunzi, anwani, namba ya kitambulisho au ya pasi, na tarehe ya kuzaliwa.

 2. Picha ya mwanafunzi, ishikizwe kwenye ukurasa na gundi, na ipigwe mhuri ukingoni.

 3. Jina na tarehe za kufanyika kozi hiyo.

 4. Mahali kozi ilipofanyikia, jina la kiongozi wa kozi au la Mkuu wa Shule.

 5. Jina na anwani ya msimamizi wa mwanafunzi.

 6. Orodha ya masomo yaliyosomwa. Hapo chini pana orodha iliyoandaliwa tayari kwa kunakiliwa.

 7. Uthibitisho wa idadi ya insha zilizoandikwa na alama zilizopatikana.

 8. Uthibitisho wa idadi ya mazoezi ya vitendo yaliyofanywa.

 9. Tarehe ya kufanyika mtihani na matokeo.

 10. Chanzo cha masomo ya kufundishia ni Dk. Les Norman, Th.D, M.Ph, DCI World Christians, PO Box 5091, Nottingham NG25 0DH, England.

 11. Ukadiriaji wa kitaaluma.

 

Hili litaeleweka na Chuo cha Elimu ya Juu au Chuo Kikuu ambavyo vina hiari ya kukataa au kukubali sifa hizo za kitaaluma katika kumfikiria mwanafunzi anayewania kuchukua kozi katika chuo chao. Ieleweke wazi kwamba hatuwezi kumhakikishia mwanafunzi ye yote kwamba chuo cho chote kitavikubali vyeti vyetu au vya vyuo vingine vyo vyote. Hata hivyo vyuo vingi vitayakubali masomo yetu na hasa vyeti vinapokuwa vimeambatana na hati za maelezo.

 

"Dk. Les Norman, Th.D, M.Ph, wa mtandao wa DCI wa Wakristo wa Ulimwengu mzima aliyeko Uingereza, anathibitisha kwamba kama kozi hii ingefanyika kwenye majengo yao na chini ya uangalizi wao muda halisi wa darasani na kusoma ungekuwa kama ifuatavyo:

 

Masomo 85 kwa muda wa saa 1½ wa darasani  kila somo = masaa 127.5.

Mazoezi 85 ya kuandika kwa muda wa masaa 3 kila zoezi  = masaa 255.

Mazoezi 85 ya vitendo kwa muda wa masaa 2 kila zoezi    = masaa 170. Jumla ya masaa yote ni 552.

Masaa hayo 552 ni sawa na krediti-saa 34.

 

Kwahiyo thaminisho la kitaaluma la Cheti cha Masomo haya ya Biblia ni  krediti 34 za muhula."

 

Sehemu hii ya mwisho ilikuwa ni kwa ajili ya Viongozi wa Shule za Biblia, Umisheni na Kanisa ambao wamefuatwa na mwanafunzi au msimamizi wake wakiomba kibali na utetezi kwa ajili ya kozi anayotarajia kusoma mwanafunzi, na kwa matumaini kwamba kanisa, misheni, shule au taasisi itatoa stashahada mwishoni mwa kozi na baada ya kufaulu mtihani.

 

Tafadhali mwandikie Dk Les Norman kwa ajili ya kupata ushauri na maelezo zaidi: support@dci.org.uk

 

Je, Stashahada yaweza kuwa na krediti za kitaaluma?

Inakuwa vigumu kutoa hakikisho kwamba taasisi yo yote ya kitaaluma itavikubali vyeti kutoka nje, lakini vyuo vingi hakika vitaifikiria kazi iliyothibitishwa. Kwa mfano, stashahada halali iliyotolewa kutokana na masomo yetu itakubaliwa na taasisi ya New Covenant International University nchini Marekani katika maombi ya krediti kwa ajili ya kujiunga na masomo ya juu katika chuo chao. Taasisi hiyo inayo tovuti yake na barua-pepe kwa ajili ya mawasiliano kwa lugha ya Kiingereza hapa: www.newcovenant.edu

 

Je, wahitimu huwa wachungaji moja kwa moja?

Uchungaji ni karama itokayo kwa Mungu ikaonekana na kutambuliwa, na wala si daraja au cheo apokeacho mtu kutoka kwa wanadamu.

 

Je, wanafunzi wako wamefanya mazoezi ya kuandika, mazoezi kwa vitendo na mtihani? Hao wanafunzi wanapaswa kufikiri, kuomba, kuandika na kutenda kama Yesu. Tafadhali usiwakubali kama wahitimu, wala kuwapa daraja la Uchungaji wanafunzi waliofanya mtihani wa darasani peke yake. Waache watambuliwe na kanisa kwa kutenda yale Yesu aliyotenda. 

 

Je, tunaweza kupata stashahada kutoka Uingereza?
Kila Shule ya Umisheni inapaswa kuandaa stashahada yake na kwa lugha yake, na kusainiwa na viongozi wa eneo hilo na ambao wanaweza kupatikana kirahisi katika kuthibitisha uhalali wa stashahada inapobidi. Pengine itakuwa vigumu kuamini kwamba mchungaji wa kijijini, tena ndani ndani kabisa, anaweza kuwa na stashahada halisi kutoka Uingereza! Kwahiyo saini za viongozi wa eneo hilo wanaofahamika ni muhimu sana.

 

Je, kuna ulazima wo wote wa kuwasimamia wanafunzi na hata kuwapa mtihani?

Ndiyo – iwapo kanisa au Shule ya Biblia ingependa kutoa stashahada ya maana na ya kuaminika mwishoni mwa kozi. Utahitaji kutunza kumbukumbu zako vizuri ili uweze kuthibitisha maulizo yo yote baadaye kuhusiana na mwanafunzi; kwa mfano kutoka kwa mwajiri, au chuoni.  

 

Hapana – ikiwa watu wameamua kujisomea masomo haya kwa furaha yao na kwa ajili ya ukuaji wa kiroho katika vipindi vya kujifunza Biblia kanisani kwao.

 

Tutafanyaje kama hatuna wasimamizi wa kutosha kanisani kwetu?

Kwanini msifikirie uwezekano wa kupata msaada kutoka kwa kanisa lingine, na pengine dhehebu tofauti na la kwenu? Kufanya kazi na makanisa mengine ni vizuri sana, na upo usemi usemao, chuma hunoa chuma. Wastaafu walio wengi kama vile wachungaji, wamishenari na wengineo watakuwa tayari kusaidia.

 

Je,  kwa namna gani shule yetu au kanisa letu linaweza kutoa vyeti vya kuaminika ?

Ikiwa wewe ni kiongozi wa shule au wa kanisa angalia ukurasa wenye taarifa za kutosha kuhusiana na swali lako.

 

Je, naweza kuanzisha shule yangu na kuipa jina la Shule ya DCI?

Asante kwa imani uliyonayo kwetu, lakini kwa sababu za kisheria itakuwa vigumu. Ingekuwa vizuri kama utabuni jina lingine na kwa lugha yenu. Kutumia jina la mtandao huu bila kibali na ruhusa kunaweza kukakuletea matatizo yasiyokuwa ya lazima. Hata hivyo unaweza ukasema kwamba masomo unayotumia kufundishia yanatolewa na taasisi ya DCI Trust ya Uingereza.

 

Maalum Kwa Walimu Na Wasimamizi:

Msimamizi anatakiwa kufanya nini?

Kazi ya msimamizi ni kusoma na kusahihisha mazoezi ya mwanafunzi, na zaidi sana aoneshe moyo wa urafiki kwa mwanafunzi wake. 

Wasimamizi wanapaswa kutoa taarifa zao kwa mchungaji au kiongozi inapofikia mwisho wa kozi. Watatakiwa kutunza kumbukumbu hizi rahisi na muhimu:

(1) Rejesta ya masomo aliyomaliza kusoma mwanafunzi, tarehe na saini ya kuonesha kwamba ameridhika na jinsi mwanafunzi huyo alivyojifunza.

(2) Rejesta ya mazoezi ya kuandika ambayo ni sehemu ya hii kozi, tarehe na maoni kuhusu ukubwa na ubora wa kazi yenyewe. Mwanafunzi atatakiwa kutunza vizuri kazi zake kwa matumizi ya baadaye iwapo zitahitajika. 

 

Huu hapa ni mwongozo wa kusahihisha:

Kwa kuwa kozi hii inasomwa maeneo mbalimbali ya ulimwengu miongoni mwa watu wanaotumia Kiingereza kama lugha yao ya pili au pengine ya tatu, tumeandaa mpango ulio rahisi wa kusahihisha. Mpango huu unaweza kutumiwa pia katika kusahihishia mitihani.

 

A = 80% -100% Kwa kweli ni kwa kazi nzuri kwa viwango vya juu sana, alama hizi hazipatikani kirahisi. Wasimamizi watatoa A au A+ kwa kazi hizo; la sivyo hakuna namna nyingine ya kuwatuza wanafunzi kama hao.

B = 70% - 79% Kazi nzuri sana, mwanafunzi amelielewa somo vizuri.

C = 50% - 69% Kazi ya wastani, angeweza kufanya vizuri zaidi.

D = 50% na pungufu ya hapo. Mwanafunzi atatakiwa kurudia somo au mtihani ili aweze kuipata maana.

 

Kila daraja linaweza pia kuwa na alama + au -, kwa mfano B- au C+.

 

(3) Kumbukumbu za lengo na matokeo ya mazoezi ya vitendo yakiwa na jina na tarehe. Hatuangalii mafanikio ya papo kwa papo kila mara, lakini pana uzoefu wa kujifunza kila mara panapokuwepo na kuwafikia watu.

 

Na insha zinasahihishwaje na kuwekewa alama kama A, B, C nk.? 

Kwanza angalia urefu wa kazi yenyewe, kwangu mimi maneno 350/400 ni sawa na ukurasa mmoja. Kisha angalia kama mwanafunzi anajibu swali aliloulizwa, isije ikawa amejibu harakaharaka bila kuelewa. Halafu angalia kama jibu la mwanafunzi halivuki mipaka ya somo; na halafu angalia ukweli, usahihi na uwasilishaji, unadhifu na usomekaji. Waweza kumwona mwalimu wa shule ya sekondari akakushauri njia sahihi ya kutathmini kazi. Baadhi ya tamaduni huweka thamani kubwa zaidi kwa baadhi ya mambo kuliko mengine na ni muhimu kulielewa hilo na mambo yenyewe.

 

Mtihani wenyewe uko wapi?

Mtihani unapatikana kwenye mtandao; kuna maelekezo kwenye tovuti yatakayokuwezesha kuuona mtihani ulipo mwishoni mwa kila sehemu na kila somo. Utaratibu wa kusahihisha ni kama ulivyoelezwa hapo juu. Mwishoni mwa kozi msimamizi anaweza akaomba jalada lenye majibu. Utakapofanya hivyo tafadhali wasiliana nasi kwa baruapepe ukitushirikisha pia jina lako kamili, anwani yako, umri wako, namba ya kitambulisho au pasi yako, namba ya simu yako, jina la mchungaji wako, jina la kanisa na anwani; na taarifa kama hizo kwa ajili ya mwanafunzi wako. Asante.

 

Kunatokea nini mwishoni mwa kozi?

Mwishoni mwa masomo, msimamizi atawasilisha kwa mchungaji au kiongozi, ambaye hapo awali aliidhinisha kozi hiyo pamoja na stashahada, rejesta, kumbukumbu na sampuli za kazi za mwanafunzi.  Mchungaji au kiongozi atazipitia na kuidhinisha yafuatayo: 

 1. Aina tatu za kumbukumbu kama zilivyoelezwa hapo juu pamoja na maoni na mapendekezo ya msimamizi.

 2. Matokeo ya mtihani.

 3. Tabia ya mwanafunzi na ridhaa yake wakati wa kozi.

 

Wakati mwingine atataka kumsaili huyo mwanafunzi. Kwa kawaida stashahada hutolewa katika Sherehe za Mahafali ambapo kanisa lote, familia na marafiki hualikwa kuhudhuria. Tungependa kwamba kila mwanafunzi atamke hadharani maono yake kwa huduma iliyoko mbele yake.

 

3. MASWALI ZAIDI NA MAJIBU ZAIDI

 

DCI ina maana gani?

DCI inajumuisha shughuli zinazofanywa na kundi la watu katika mataifa mbalimbali kwenye taasisi ya The DCI Foundation, Shule za Umisheni, Kurasa za Habari za Wakristo wa Ulimwengu wote na tovuti hii. Jina lenyewe linatokana na andiko la Warumi 1:1 katika Biblia pale ambapo Paulo katika lugha ya awali anajitambulisha mwenyewe kama Doulos Christou Iesou – yaani mtumwa wa Yesu Kristo. Jina hilo ambalo limeanza kutumika tangu mwaka 1986 linatukumbusha nafasi yetu na wito wetu wa kumtumikia Bwana na ulimwengu wa watu.

 

Ninyi ni akina nani na mnatokea wapi?

Angalia habari zetu hapa www.dci.org.uk Mkurugenzi wa masomo haya ni Dk. Les Norman, Th.D, Ph.M mwenye uzoefu wa zaidi ya miaka 30 katika huduma za kikristo. Sisi tupo Uingereza, na katika kupunguza gharama tunafanyia kazi majumbani mwetu na tunaishi maisha ya kawaida. Watendakazi pamoja nasi na wanafunzi wanatoka sehemu mbalimbali ulimwenguni kote.

 

Je, ninyi ni wa dhehebu gani?

Taasisi hii ya DCI imeamua kwa makusudi kabisa kutokuwa chini ya dhehebu lo lote moja, na watu wanaofanya kazi pamoja katika mtandao huu wa umisheni wanatoka kwenye madhehebu mbalimbali ya kikristo kutoka mataifa mbalimbali. Kitaaluma sisi tumeshirikishwa na Chuo Kikuu cha NCI cha Marekani ambapo Dk. Les Norman anatambuliwa kama  profesa mshiriki. Na hapa Uingereza Mkurugenzi huyu pamoja na nyumba yake ni washirika katika kanisa moja la kiinjili linalokua; na watendakazi wengine wapo kwenye makanisa kama hilo, makubwa au madogo, lakini madhehebu tofauti tofauti.

 

Je, mna tamko lo lote la imani?

Sisi tunakubaliana na Imani ya Nikea ya mwaka 381 BK au Imani ya Mitume ya kanisa la kwanza ambayo inatambuliwa na kutumika kama mfano kwa kanisa na vikundi vya Kikristo ulimwenguni mwote..

"Tunamwamini Mungu mmoja, Baba, Mwenyezi, mwumba wa mbingu na nchi, na vyote vilivyopo, vinavyoonekana na visivyoonekana. Tunamwamini Bwana mmoja, Yesu Kristo, mwana pekee wa Mungu, aliyetoka kwa Baba, Mungu kutoka kwa Mungu, Nuru kutoka kwa Nuru, Mungu wa kweli kutoka kwa Mungu wa kweli, aliyetoka kwa Mungu, hakuumbwa, mwenye asili moja na Baba. Kwa kupitia kwake vitu vyote viliumbwa. Kwa ajili yetu na kwa wokovu wetu alitujia kutoka mbinguni: kwa uweza wa Roho Mtakatifu alipokea mwili kutoka kwa Bikira Maria, na akafanyika mwanadamu. Kwa ajili yetu alisulibiwa chini ya Pontio Pilato; akafa na kuzikwa. Siku ya tatu akafufuka kwa mujibu wa Maandiko; akapaa mbinguni na ameketi mkono wa kuume wa Baba. Atakuja tena katika utukufu kuwahukumu walio hai na wafu, na ufalme wake hautakuwa na mwisho. Tunamwamini Roho Mtakatifu, Bwana, mtoa uzima, atokaye kwa Baba na Mwana. Yeye pamoja na Baba na Mwana huabudiwa na kutukuzwa. Alinena kupitia Manabii. Tunaamini katika kanisa moja takatifu, katoliki na la kitume. Tunakiri ubatizo mmoja kwa msamaha wa dhambi. Tunatazamia kufufuliwa kwa wafu, na uzima katika ulimwengu ujao."

(Neno "katoliki" lina maana ya kanisa la ulimwengu mzima la Bwana Yesu Kristo).

 

Je, kuna namna ninavyoweza kuwasaidia ninyi kwa haya mnayoyafanya?

Tunakushukuru sana kwa wazo hilo. Kwa kweli tunathamini sana kila msaada tunaopewa kwa sababu hatutozi ada yo yote ama kwa masomo ya kwenye mtandao wa kompyuta au kihistoria katika shule zetu. Mara kwa mara pia tunatoa misaada ya kuwategemeza watu wengi na miradi katika misheni na katika kazi miongoni mwa watu maskini. Hatupewi misaada ya kidhehebu wala udhamini wa mashirika, na wala hatujitangazi katika tovuti yetu. Sasa iwapo umebarikiwa na hii Shule ya Umisheni, tutashukuru kupokea kutoka kwako matoleo yatakayotupa sisi uwezo zaidi wa kuendelea kutoa mafunzo haya bila malipo kwa watu wengine wengi zaidi katika nchi zinazoendelea kwa sababu uwezo wao wa kulipia gharama za masomo haya ni mdogo. Tutaweza pia kuwawezesha wahitimu wetu na viongozi kuanzisha misheni mpya au miradi ya kujikimu.

 

Je, ni lugha gani nyingine mnazotumia?

Angalia ukurasa wetu wa kwanza hapa www.dci.org.uk na utagundua kwamba zipo lugha nyingine nazo ni Kiingereza, Kihispania, Kireno, Kisebuano, Kijerumani, Kiarabu, Kihindi, Kiindonesia, Kimori, Kirumania, Kirusi, Kiswahili, Kitelegu, na Kichina. Tunakaribisha watu wa kujitolea wajiunge na timu yetu katika kutafsiri masomo haya kwa lugha nyingine zaidi.

 

Ni masomo gani yapewe kipaumbele kwenye kongamano la viongozi katika nchi zinazoendelea?

Kama utakuwa na muda wa kutosha kwa masomo saba, na iwapo watu wameshaelewa mambo ya msingi, basi tunapendekeza mada zifuatazo kutoka kwenye orodha ya masomo ya umisheni: 11.Mpango wa Mungu kwa Ulimwengu; 12.Agizo Kuu; 38.Mrejeshe Mfalme; 63.Kulijenga Kanisa; 64.Kanisa la Mavuno; 65.Kanisa la Utumishi; 66.Kanisa la Ushuhudiaji.

 

Je, naweza kutoa nakala za masomo yenu kwa ajili ya wengine?
Ndiyo, unaweza kufanya hivyo na kutoa kwa wengine kila kitu ulichopokea kutoka kwetu. Unakaribishwa. Hatutakutoza cho chote kwa habari ya hatimiliki ilimradi unatoa bure kama nasi tulivyokupa bure, ila gharama utakazotoza wewe ni zile gharama halisi za kutolea nakala hizo.

 

© The DCI Foundation, England

Taasisi inayotegemeza umisheni ulimwenguni tangu mwaka 1985

 

Tovuti ya Shule za Umisheni  ya DCI

www.dci.org.uk

 

Anwani kwa Mawasiliano

support@dci.org.uk

  
 1985 - 2008

With many thanks to Pastor Dastan Mboera, Dar es Salaaam, Tanzania
and EAPTC Nairobi, Kenya for this revision and translation from the original English.
mboeradsk @ yahoo.com


© Dr Les Norman  The DCI Trust, UK
Permission is granted to provide copies at cost price for study purposes
but not for sale or commercial purposes. Freely you have received, so please freely give.

Karibu Kwenye Shule Ya Umisheni Katika Lugha Ya Kiswahili
Support Pages in English


www.dci.org.uk