1985 - 2007


3. Mwulize Mungu
Ni Maombi Gani Yanayoweza Kuwaleta Wenye Dhambi Kwa Yesu?

Support Pages   Index To All Lessons   School of Finances  
World Christian News   
Who Are We?   Site Index

 

Soma Haya Katika Biblia Yako

Ezekieli 34

 

Mstari Wa Kukariri

Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho (Efe 6:12).

 

Baadaye Fanya Yafuatayo

Yafaa sana leo utafute muda ili kufanya maombi kuhusiana na yale mambo tuliyojifunza kwa pamoja.


Jambo La Kufanya Kabla Hatujakutana Tena

Tafuta muda mzuri wa kufanya maombi na maombezi kwa ajili ya mahitaji yako/yenu ya kiroho. Tunahitaji maombi ili tuweze kuwa mashahidi hodari wa Yesu.

 

Kazi Ya Kuandika Ya Stashahada

Andika maombi yasiyozidi kurasa mbili, ukifanya maombezi sawasawa na andiko la 1Tim 2:1-8 kwa ajili ya viongozi wa ngazi mbalimbali na kwa ajili ya watu wa taifa lako.

 

Tafakari Andiko Lifuatalo Neno Kwa Neno

Matendo 26:28,29

 

Tumia Muda Wa Dakika Moja Kuubadilisha Ulimwengu

Omba kwa ajili ya taifa la Algeria. Idadi ya watu: 30,000,000. Idadi ya Waislamu: 99.4%. Wote hawajafikiwa; kuna upinzani mkubwa dhidi ya Injili.

 

 

Hakikisha umewafundisha wengine somo hili.
Kila mara omba na kujiandaa ukiongezea mistari mingine ya Biblia
na mifano yako mwenyewe ili kufanya somo lieleweke vizuri zaidi.
 


Umati Wa Watu

Siku moja niliingia sokoni na kukuta msongamano mkubwa wa watu wakisukumana katika kutafuta huduma, nusura wanigonge. Mwanzoni nilijisikia vibaya na kuwawazia vibaya watu wale kwa sababu walikuwa wakisukumana, wakipiga kelele, hali wengine wanakunywa, na wengine wengi wakivuta sigara, na kutumia lugha chafu.  Mara nikakumbuka kwamba Yesu naye alikutana na watu kama hao, lakini Yeye hakuwakasirikia kwa sababu aliwaona kama watu waliobughudhiwa na wasio na msaada. Yesu aliwahurumia na kuwataka rafiki zake, yaani wafuasi wake, waombe ili wapatikane watendakazi wa kuwasaidia watu hawa
(Mt 9:35-38).                                                     

Kondoo Wasio Na Mchungaji

Baada ya kukumbuka habari za Yesu nilitubu kwa kukosa uvumilivu juu ya watu wale; na nikaanza kuomba. Nilihisi kama Mungu alikuwa anazungumza na moyo wangu akisema, “Ikiwa kweli unataka kuwasaidia watu hawa, hakuna juhudi za kibinadamu zinazoweza kuzaa matunda. Jambo la maana ni kwa wewe kunikaribia kwa maombi; nami nitajibu maombi yako kwa kuwavuta watu hao kwangu”.

Maombi Ya Biblia Yanayoweza Kuokoa Waliopotea

Hebu fikiri kidogo, halafu uone kama kuna mifano, katika Biblia, ya maombi ya kumsihi Mungu awaokoe watu kama vile baba, mama,  ndugu, rafiki, nk. Jibu ni kwamba hakuna maombi kama hayo!

Kwa nini?

Ni kwa sababu Mungu mwenyewe alishaonesha nia ya kutaka watu wote waokolewe. Yeye amejitoa kwa ajili ya suala la wokovu na ana nia kuliko sisi. Kwake Yeye suala la wokovu ni jambo ambalo tayari lilishafanyiwa uamuzi, na ni uamuzi wa kudumu. Hakuna mjadala kama aokoe au asiokoe.

Mungu aliweka ahadi ya kumponda nyoka kichwa, yaani mamlaka ya Shetani (Mwa 3:15)

Mungu alijifunga mwenyewe katika maagano ya kumbariki mwanadamu                                     (Mwa 9:1-17) (Mwa 15 na 17) (Kut 34:10)

Ingawa mwanadamu alilivunja agano mara kwa mara, Mungu katika upendo wake na huruma yake, aliahidi agano jipya katika Yer 31:31.

Alimwahidi Ibrahimu kwamba kwa kupitia kwake, na kwa imani, jamaa zote za ulimwengu watabarikiwa. (Mwa 12:1-3).

Mungu aliwapa taifa lote la Israeli kazi ya kuhudumu baraka zake hapa duniani (Kut 19:5,6).

Katika Ezekieli 34 mistari ya 4,12 na 16, Baba anaonesha huruma yake kuu kwa kuazimia kwamba hata kama mwanadamu hataonesha kujali, Yeye mwenyewe atawatafuta waliopotea, na walioiacha njia atawarejesha; atawaganga waliojeruhiwa, na kuwatia nguvu walio dhaifu.

Zaidi ya yote Mungu alimtuma Mwanaye Yesu ili atafute na kuokoa waliopotea.
(Lk 19:10) (Lk 4:18).

Wakati Mungu alipomtuma Roho Mtakatifu, kitu cha kwanza alichokifanya hadharani ni kuwajulisha watu waliotoka sehemu mbalimbali za ulimwengu wote, na kwa lugha zao wenyewe, maajabu ya Mungu. (Mdo 2:1-12).                                                   

Je, Ni Sala Ipi Bora Kuliko Zote Katika Biblia?

Kwa kuwa sasa tunajua jinsi Mungu alivyojitoa na kumaanisha, tunaweza kuomba kwa Jina la Yesu tukiwa na huruma, uvumilivu, msisitizo na kwa kujiamini: “ Ufalme wako uje, mapenzi yako yatimizwe hapa duniani, kama huko mbinguni. Amen”.

Tuombeje Basi?

Ingawa tumejua kwamba Mungu amejitoa na kwa kumaanisha kutaka watu waokolewe, lakini bado ni jukumu letu kuomba mara kwa mara katika uvumilivu na kwa kuwaonea huruma waliopotea. Sasa tuombe nini?

Kwanza lazima tujiombee wenyewe;

ili nia zetu ziweze kuona ukweli wa upotevu (Ufu 20:11).

Pia tuweze kuwahurumia waliopotea (Lk 19:10). 

Tuombe ili Mungu afungue milango (1 Kor 16:9) (2 Kor 2:12) (Mdo 14:27) (Kol 4:3) (Ufu 3:8).

Tuombe ili tuweze kufuata maongozi ya Mungu. (Mdo 8:26-).

 

Tuombe hekima ya Mungu, maana yawezekana fursa isipatikane pale tunapotazamia, kwa kuwa mara kwa mara tumekuwa tukiona au kutenda kwa makosa. (Yak 1:5).

Tuombe kupata ujasiri. (Efe 6:19) (Mdo 4:29).

Tuombe kwa ajili ya uhuru wa Roho Mtakatifu kufanya kazi ya kuwashuhudia watu kwa habari ya dhambi. (Mdo 1:8).

Tuombe kwa ajili ya maneno Yake. (Isa 59:21) (Yer 1:9).

Tuombe kwamba mawazo yetu na misimamo yetu na dhana nzima iwe ni katika kupanda na kuvuna. (Mt 13:1-23) (Isa 53:10,11).

 

Lazima Tuwaombee Watu Mara Kwa Mara

Maombi yanadhihirisha upendo wetu. Maombi mazuri kabisa ni pale tunapochukua yaliyo matakwa ya Mungu na kuyapeleka tena mbele zake kwa njia ya maneno. Paulo anatuelekeza namna ya kuombea watu katika 1Tim 2:1-3. Soma pia 1Sam 12:23.

Maombi Ni Vita Vya Kiroho

Ijapokuwa mungu wa ulimwengu huu, Shetani, amezitia giza akili za wasioamini, maombi yatafungua macho hayo yasiyoona na kuwaokoa watu kutoka katika nguvu za Shetani ili kwamba wapate kusamehewa na kujiunga na jamaa ya Mungu (2Kor 4:4) (Mdo 26:18). Ni lazima tuombe dhidi ya kazi ya Shetani ya kuwazuia watu wasimwamini Yesu; pia tumwombe Mungu atupatie fedha na nyenzo nyingine kwa ajili ya kupeleka Injili kwa walengwa (Efe 6:12). Kwa kweli Shetani amewakamata watu kwa nguvu kiasi kwamba Yesu alituagiza tumwombe Mungu apeleke watendakazi zaidi shambani kwa kazi ya kuvuna, yaani Mungu aweke msukumo kuwezesha kazi hiyo kufanyika (2Kor 2:11) (Mt 9:38).

Maombi Yaliyojibiwa

Biblia inatuambia kwamba kanisa la kwanza waliomba, na Mungu akaongeza idadi yao kila siku. Kwa kuwa viongozi wao waliona umuhimu wa maombi na Neno, idadi ya waamini wapya iliongezeka kwa kasi.(Mdo 2:42,47)(Mdo 6:4-7).

Kumbuka, kama tukiomba sawasawa na mapenzi ya Mungu, majibu yako njiani yanakuja. (1Yoh 5:14,15) (Mk 11:24) (Mt 18:19) (Mt 7:7) (Yer 33:3).


Kwa Kumalizia Omba Kwa Ajili Ya Watu Wa Ulimwengu
Huu Ambao Bado Hawajafikiwa Na Injili; Wataje Kwa Majina

Afghanistan (2)

Jina la Watu

Lugha Yao

Idadi Yao

Nangalami (Nigalami)

Grangali

24,000

Pashayi, Southwest

Pashayi,

108,000

Shughni

Shughni

10,000

Tangshewi

Tangshewi

10,000

 

 


 1985 - 2007

With many thanks to Pastor Dastan Mboera, Dar es Salaaam, Tanzania
for this revision and translation from the original English
mboeradsk @ yahoo.com


© Dr Les Norman  The DCI Trust, UK
Permission is granted to provide copies at cost price for study purposes
but not for sale or commercial purposes. Freely you have received, so please freely give.

Support Pages   Index To All Lessons   School of Finances  

World Christian News   
Who Are We?   Site Index